Kikosi cha Simba leo kimefanya mazoezi kwenye uwanja wa Uhuru kuelekea mchezo wa mkondo wa pili hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Mighty Wonderers. Mchezo huo utapigwa siku ya Jumapili, Septemba 13 katika uwanja huo.
Vijana wa kocha Steve Barker wamekamilisha mazoezi yao katika uwanja huo kwani kesho kikosi kinatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wake wa Mo Simba Arena huku Mighty Wonderers wakitarajiwa kufanya mazoezi katika dimba la Uhuru saa 10 jioni kwa mujibu wa kanuni.
Dimba la Uhuru limefanyiwa maboresho makubwa hasa katika eneo la kuchezea 'pitch' hivyo kuwapa nafasi nzuri Wana Lunyasi kuweka soka chini katika mchezo ambao Wekundu wa Msimbazi watahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare kutinga hatua inayofuata.
Wapinzani wao Mighty Wonderers tayari wamewasili nchini ambapo timu hiyo iliwasili Alhamisi usiku.
Mchezo baina ya timu hizo utapigwa Jumapili saa 10 jioni..