Klabu ya Simba leo itashuka kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuikabili Mighty Wanderers ya Malawi, katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Wekundu wa Msimbazi watashuka dimba la Uhuru wakiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa nchini Malawi, shukrani kwa goli lililofungwa na Anicet Oura.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ili kujihakikishia nafasi ya kutinga raundi inayofuata ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker jana aliweka wazi dhamira yake ni kuona vijana wake wakiibuka na ushindi mnono mbele ya mashabiki wao huku akiwataka wachezaji kutobweteka na ushindi wa ugenini.
Barker amewataka wachezaji wa Simba wacheze kwa nidhamu ya hali ya juu ili kulinda heshima ya klabu nyumbani na kuendeleza rekodi yao nzuri kwenye michuano ya CAF.
Hali ya morali ya Wekundu hao wa Msimbazi iko juu, huku wachezaji wakichochewa zaidi na motisha ya kifedha kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo ambapo Rais wa heshima wa Simba Bilionea Mohamed Dewji amewawekea mezani Tsh Milioni 200.
Kwa upande wao, Mighty Wanderers watahitaji muujiza kupindua meza dimba la Uhuru. Timu hiyo itahitaji kufunga angalau mabao mawili na kuibuka na ushindi ili kusonga mbele.
Habari njema kwa Simba ni kurejea kikosini kwa kiungo mshambuliaji Libasse Gueye ambaye amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye michuano hiyo msimu uliopita.
Gueye amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Simba msimu huu akihusika katika mabao 6 kati ya 9 yaliyofungwa na Simba kwenye ligi.