Klabu ya Simba SC leo inashuka kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kukabiliana na FC 15 de Agosto kutoka Equatorial Guinea, katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL).
Mchezo huu unatazamwa kama wa kukamilisha ratiba kufuatia ushindi mnene wa mabao 6-1 uliopatikana kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Jumatano iliyopita dimba la Uhuru.
Ushindi huo unaifanya Simba kuingia uwanjani ikiwa na mtaji mkubwa wa mabao matano, hatua inayoweka mguu mmoja wa Wekundu wa Msimbazi kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa vilabu barani Afrika.
Licha ya ushindi wa mabao 6-1 kwenye mchezo wa kwanza, kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo hayo na badala yake kukamilisha kazi hiyo kwa nidhamu ya hali ya juu mbele ya mashabiki wao.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ali, amesisitiza kuwa malengo ya klabu msimu huu ni makubwa, wakilenga kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Ahmed amesema dhamira yao ni kutinga hatua ya makundi kwa ushindi wa kihistoria ili kupeleka ujumbe kwa wapinzani wao.