Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo ambapo vinara wa ligi hiyo Simba Sc wako mkoani Manyara kuikabili Fountain Gate.
Ni katika mchezo unaotarajiwa kupigwa saa 10 jioni kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
Vijana wa kocha Steve Barker watakuwa na nafasi ya kujiimarisha zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi kama wataondoka na alama zote tatu.
Msimu huu Simba imeweka rekodi ya aina yake ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo ikiandikisha ushindi wa asilimia 100 katika mechi 8.
Hii itakuwa mara ya pili kucheza dimba la Tanzanite Kwaraa Wanamsimbazi wakikumbuka kudondosha alama 2 mara ya mwisho walipocheza hapo misimu miwili iliyopita.
Hata hivyo msimu huu Simba iko kwenye kiwango bora na pengine Fountain Gate pamoja na kuwa bora, watahitaji bahati kuwa upande wao ili kuweza kupata chochote mbele ya Simba.