Jana Simba ilishinda mechi yake ya tisa mfululizo kwenye ligi kuu ya NBC msimu huu wakiichapa Fountain Gate bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
Ni mwendelezo wa rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 msimu huu, kwani Mnyama amechukua alama 3 kwenye kila mchezo wa ligi.
Lakini pia ulikuwa mchezo wa 19 mfululizo wa ligi Simba inashinda. Ikumbukwe mara ya mwisho Simba kudondosha alama kwenye ligi ilikuwa mchezo dhidi ya Yanga msimu uliopita uliopigwa uwanja wa Isamuhyo na kumalizika kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2.
Tangu wakati huo hakuna timu iliyoweza kuondoka na alama yoyote mbele ya Mnyama ambaye ni wazi msimu huu amedhihirisha mapema ubingwa ni halali yake.
Katika mashindano yote Simba pia imeshinda mechi 13 mfululizo, mechi 9 za ligi na mechi nne za hatua ya awali ya ligi ya mabingwa.
Simba inafukuzia rekodi ya kushinda mechi 14 mfululizo na wataifikia kama wataibuka na ushindi dhidi ya Namungo Fc katika mchezo wa ligi utakaofuata utakaopigwa Novemba 02 uwanja wa Uhuru.