Ushindi wa mabao 3-2 walioupata Simba SC dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Uhuru juzi unaweza kuwa umewapa alama tatu muhimu na kuendeleza rekodi ya ushindi wa asilimia 100 msimu huu, lakini umeliacha benchi la ufundi na kazi ya kufanya hasa aneo safu ya ulinzi pale anapokosekana beki Ismail Toure.
Mchezo huo ambao Simba iliruhusu mabao mawili kwa mara ya kwanza msimu huu, umedhihirisha Toure ndiye kila kitu na muhimili mkuu wa safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi kwa sasa.
Yeye na Rushine de Reuck wametengeneza pacha imara kwa kuwa wamecheza mechi nyingi pamoja. Ziko nyakati Rushine alikosekana Toure akatumika sambamba na Yusuph Kagoma lakini juzi alipokosekana Toure mambo yalikuwa tofauti.
Katika mchezo huo, mkufunzi wa Simba Steve Barker alimuanzisha Ibrahim Nindi kuziba nafasi ya Toure na kucheza pacha wa ulinzi na Rushine De Reuck. Hata hivyo, wawili hao walionekana kukosa kabisa maelewano na kucheza eneo moja mara kwa mara.
Udhaifu huo wa mawasiliano ulimpa mwanya mshambuliaji wa Namungo, Raymond Lulendi kuweza kuipasua ngome ya Simba na kufunga mabao mawili ya haraka.
Bila Toure, ambaye amekuwa akisifika kwa utulivu, uwezo mkubwa wa kushinda mipira ya juu, na doria za ardhini zinazookoa makosa ya mabeki wenzake, Simba ilionekana kuwa hatarini kila wakati Namungo waliposogea langoni mwao.
Bahati nzuri kwa Simba ni kwamba safu yao ya ushambuliaji ilikuwa macho na kupambana hadi sekunde ya mwisho. Winga Anicet Oura aliibuka shujaa wa mchezo huo kwa kufunga mabao mawili (dakika ya 3 na 88), huku beki De Reuck akifunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 79, na kukamilisha mapinduzi hayo ya kibabe yaliyookoa alama tatu.
Ushindi huo uliifanya Simba iweke rekodi ya kushinda mechi 20 mfululizo za ligi kuu tangu msimu uliopita huku wakishinda mechi 10 msimu huu na 10 zikiwa mechi za mwisho msimu uliopita.