Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Ahmed Ali, amesema klabu hiyo imetoa somo katika soka la Tanzania kuhusu masuala ya mikataba, akieleza kuwa si klabu pekee zinazopaswa kulipa fidia zinapovunja mikataba na wachezaji au makocha, bali hata wachezaji na makocha wanaweza kutakiwa kulipa fidia wanapovunja mikataba yao.
Ahmed ameeleza kuwa kwa muda mrefu wadau wa soka wamezoea kuona klabu zikilazimika kuwalipa wachezaji fidia baada ya kuvunja mikataba yao, huku makocha nao wakilipwa stahiki zao wanapotimuliwa kabla ya muda wa mikataba yao kumalizika.
Hata hivyo, amesema suala hilo lina upande mwingine ambao ni muhimu kwa wadau wa soka kuuelewa, kwamba mchezaji au kocha anaweza kuwajibika kulipa fidia kwa klabu anapovunja mkataba, endapo makubaliano yao yana kipengele kinachobainisha wajibu huo.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Ahmed aliandika:
"Mara nyingi tumezoea kuona wachezaji wakilipwa baada ya kuvunjiwa mkataba, au kocha akilipwa stahiki zake baada ya kutimuliwa.
"Kwa mara ya kwanza mpira wa Tanzania umepata somo kuwa kocha au mchezaji anatakiwa kulipa fidia pale anapovunja mkataba endapo mkataba wenu una kipengele hicho.
"Kaeni na sisi vizuri tuendelee kuwapa elimu ya mpira!!!!"
Ahmed ametoa kauli hiyo wakati Simba ikithibitisha kumfungulia madai FIFA kocha wao wa zamani Fadlu Davids baada ya kuvunja mkataba wake kinyume na makubaliano.
Simba inamdai Fadlu zaidi ya Tsh Milioni 100