Wakati Kamati ya uchaguzi ya TFF ikitangaza kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo hadi Januari 30, baadhi ya wanachama wa Simba wameitaka Kamati hiyo kurudisha uchaguzi Januari 3, 2027.
Hofu kubwa ya mwingiliano wa ratiba kati ya shughuli za uchaguzi na mechi muhimu za kimataifa pamoja na dabi ya watani wa jadi inatajwa kuwa sababu ya mapendekezo hayo.
Wakizungumza kwenye mkutano na wanahabari hapo jana, wanachama hao walisema kufanyika kwa uchaguzi mwishoni mwa mwezi Januari kunaelezwa kuwa kunaweza kuivuruga timu kiakili na kiufundi.
Ratiba inaonyesha kuwa kuanzia tarehe 21 Januari 2027, kutakuwa na mfululizo wa mechi ambapo miamba hiyo ya Msimbazi itakuwa uwanjani ikipambana katika mechi za ligi kuu na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), mchezo dhidi ya Orlando Pirates utakaopigwa Januari 28.
"Hatuwezi kuwa katikati ya mapambano makubwa ya Afrika huku klabu iko kwenye joto la kampeni na uchaguzi. Akili za wachezaji na viongozi zinatakiwa kuwa uwanjani, sio kwenye masanduku ya kura," alisema mmoja wa wanachama waandamizi wa klabu hiyo.
Sababu nyingine inayotajwa na wanachama hao ni maandalizi ya dabi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, inayotarajiwa kupigwa tarehe 6 Februari 2027.
Hoja iliyoibuliwa ni kuwa klabu itakuwa na wiki moja tu ya mpito chini ya uongozi mpya kabla ya dabi, jambo linaloweza kuathiri maandalizi kuelekea mchezo huo muhimu.
Lakini pia, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti Wakili Kiomoni Kibamba, ilibainisha kuwa ukomo wa kikatiba wa uongozi uliopo madarakani unamalizika rasmi kabla ya Januari 29, 2027.
Hatua ya kuweka uchaguzi tarehe 30 Januari inatajwa na wanachama hao kama ukiukwaji wa miongozo na muda wa kisheria.