Aliyewahi kuwa nyota wa Klabu ya Simba SC, Luis Miquissone, amerejea tena kwenye soka la Tanzania baada ya kujiunga na Singida Black Stars (Singida BS), akitokea Al Ahly Benghazi ya Libya.
Kiungo huyo mshambuliaji raia wa Msumbiji anarejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na historia ya kuitumikia Simba SC kwa vipindi viwili tofauti, ambapo aliweza kujitengenezea jina kubwa kutokana na uwezo wake wa kuchezea mpira, kasi na ubunifu katika safu ya ushambuliaji.
Miquissone ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni waliowahi kutamba ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, ambapo kiwango chake kizuri kilimfungulia milango ya kusajiliwa na miamba ya soka barani Afrika, Al Ahly ya Misri.
Baada ya kuondoka Simba na kujiunga na Al Ahly, nyota huyo alirejea tena Msimbazi kwa awamu ya pili, lakini safari hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani aliitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja pekee kabla ya kurejea nchini kwao Msumbiji na kujiunga na UD Songo.
Safari yake ya kisoka ilimfikisha pia katika klabu ya Al Ahly Benghazi ya Libya, ambako anatokea kabla ya kuamua kurejea Tanzania kwa mara ya tatu, safari hii akiwa na jezi ya Singida Black Stars badala ya Simba.
Miquissone ataanz kuitumikia Singida BS baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa