Kinyang'anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Klabu ya Simba SC kimezidi kupata msisimko baada ya wanachama wengine kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu leo Ijumaa, Novemba 20, 2026, ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo.
Katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam, wagombea mbalimbali wamejitokeza kuwania nafasi za Mwenyekiti na Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, huku kila mmoja akieleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya klabu hiyo ya Msimbazi.
Miongoni mwa waliojitokeza ni mwanachama wa Simba, Yusuph Omar Yenga, ambaye amechukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, akieleza kuwa ameamua kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho ili kushiriki kuleta mabadiliko na kuimarisha uendeshaji wa klabu.
Yenga amesema Simba inahitaji viongozi wenye maono mapya, hususan katika kuimarisha mifumo ya kiutawala na kifedha, huku akiahidi kushirikiana na viongozi wenzake kuisukuma klabu hiyo kufikia hatua nyingine ya maendeleo endapo atapata nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, Sam Sasali naye amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Simba, akisisitiza umuhimu wa kuingiza damu mpya na fikra tofauti katika uongozi wa klabu hiyo.
Sasali amesema pamoja na kutambua mchango wa viongozi waliopo katika maendeleo ya Simba, anaamini umefika wakati wa kuleta mawazo mapya yatakayosaidia kukabiliana na changamoto zilizopo na kuisogeza klabu mbele zaidi.
Wakati huohuo, Swedi Mkwabi, ambaye pia anawania nafasi ya Mwenyekiti, amefika mwenyewe katika ofisi za TFF na kurejesha fomu yake ya kuwania nafasi hiyo.
Mkwabi alichukua fomu hiyo jana, Alhamisi, Novemba 19, 2026, kwa njia ya mtandao kabla ya kufika leo kukamilisha hatua ya kuirejesha.
Hata hivyo, tukio jingine lililovuta hisia ni la mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio', ambaye amefika TFF kurejesha fomu ya kuwania ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na kuchukua fomu nyingine ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti.
Julio amesema amefikia uamuzi wa kuwania Uenyekiti baada ya kutomuona Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Murtaza Mangungu, akichukua fomu hadi kufikia saa nane mchana.
Nyota huyo wa zamani amesisitiza kuwa uzoefu wake wa kuitumikia Simba unampa msingi wa kuwania nafasi hiyo, akieleza kuwa uongozi hauhitaji fedha pekee, bali pia busara, maono na uwezo wa kufanya maamuzi yenye manufaa kwa klabu.
Kujitokeza kwa wagombea hao kunaongeza idadi ya wanachama wanaotaka kushika nafasi za uongozi, huku kinyang'anyiro cha Uenyekiti kikizidi kuvuta hisia kutokana na majina yaliyoweka wazi nia ya kugombea, akiwemo aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Zoezi la kuchukua na kurejesha fomu lililoanza Novemba 16, 2026, limehitimishwa leo, huku hatua inayofuata ikiwa ni kutolewa kwa orodha ya awali ya wagombea kati ya Novemba 21 na 23, kabla ya taratibu nyingine za uchaguzi kuendelea.