Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amepongeza kiwango na uimara wa kikosi chake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, akisisitiza kuwa timu yake imeonyesha uwezo wa kushinda michezo hata inapokutana na mazingira magumu.
Barker amesema ushindi huo haukuwa rahisi kutokana na upinzani mkali kutoka kwa JKT Tanzania, ambao walipambana kwa nguvu na kuifanya Simba kutumia juhudi kubwa kuhakikisha inaondoka na alama zote tatu.
Akizungumzia mchezo huo, Barker ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa walizokutana nazo ni faulo nyingi zilizokuwa zikifanywa na wapinzani wao, hali iliyokuwa ikikatiza kasi ya mchezo na kuathiri mtiririko wa mashambulizi ya Simba.
Hata hivyo, kocha huyo ameonyesha kuridhishwa na namna wachezaji wake walivyokabiliana na changamoto hizo, wakionyesha nidhamu, uvumilivu na ari ya kupambana hadi dakika ya mwisho.
Ajivunia rekodi ya ushindi 11 mfululizo
Kocha huyo amesema jambo linalompa furaha zaidi ni kuona Simba ikiendelea kudumisha kiwango chake cha ushindi licha ya kukutana na wapinzani wenye mbinu na aina tofauti za uchezaji.
Simba imefanikiwa kushinda michezo yote 11 iliyocheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ikikusanya alama 33 kati ya 33 zinazowezekana na kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tano.
Amebainisha kuwa si kila mchezo unaweza kuwa rahisi au kwenda kulingana na mipango ya benchi la ufundi, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha timu inapata matokeo yanayohitajika.
Katika mchezo huo, Simba ililazimika kutoka nyuma baada ya JKT Tanzania kupata bao la kuongoza dakika ya 10.
Hata hivyo, mabao ya Elie Mpanzu dakika ya 20 na Libasse Gueye dakika ya 34 yaliihakikishia Simba ushindi wa mabao 2-1 na kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza hata alama moja.
Licha ya JKT Tanzania kuongeza mashambulizi katika kipindi cha pili, Simba ilifanikiwa kulinda uongozi wake hadi mwisho wa mchezo.