Nyota wa Simba SC, Maema, amekiri kuwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini ni timu yenye ushindani mkubwa, lakini amesisitiza kuwa Wekundu wa Msimbazi wana uwezo wa kupambana na timu yoyote inayotua Dar es Salaam, huku akitaja ushindi katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwa jambo muhimu.
Simba inajiandaa kuikaribisha Orlando Pirates katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku Maema akiamini kuwa kucheza mbele ya mashabiki wao ni faida kubwa inayoweza kuwasaidia kuanza kampeni yao ya kimataifa kwa ushindi.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Maema amesema kikosi chao kinaendelea kujenga kujiamini kila kinapocheza, jambo ambalo linawapa matumaini ya kufanya vizuri hata dhidi ya timu zenye uzoefu mkubwa katika michuano ya Afrika.
"Tunapaswa kuendelea kuonyesha kiwango cha juu kwa uthabiti, kupambana kwa nguvu katika kila mchezo na kutokata tamaa. Lengo letu ni kuendelea kuwapa furaha mashabiki wetu," amesema Maema.
Nyota huyo amesisitiza kuwa Simba inatambua ukubwa wa Orlando Pirates, lakini hilo haliwafanyi kuingia uwanjani wakiwa na hofu, badala yake wanahitaji kutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani.
"Kuanzia mchezo wetu wa kwanza nyumbani dhidi ya Orlando Pirates ni faida kubwa. Ni timu yenye ushindani na mabingwa nchini Afrika Kusini," amesema.
Kwa mujibu wa Maema, kucheza mchezo wa kwanza mbele ya mashabiki wa Simba ni nafasi muhimu kwa timu hiyo kuweka msingi mzuri wa safari yake katika hatua ya makundi.
Amesema licha ya kutambua kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika inawakutanisha wachezaji na timu bora zaidi barani Afrika, Simba inaendelea kupata kujiamini kupitia kila mchezo inaocheza.
"Ligi ya Mabingwa Afrika inawakutanisha walio bora zaidi, hivyo haitakuwa rahisi. Lakini tunazidi kujiamini kila mchezo unapopita. Tunahitaji pointi tatu ili kuanza kampeni yetu vizuri," amesema Maema.
Kauli hiyo inaonyesha dhamira ya Simba ya kutotaka kupoteza pointi katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi, hasa ikizingatiwa kuwa ushindi wa nyumbani unaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika mbio za kusaka nafasi ya kufuzu hatua inayofuata.