Tuanze kuisaka robo fainali kwa ushindi dhidi ya Orlando Pirates - Ahmed Ali

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
•
4h ago
Tuanze kuisaka robo fainali kwa ushindi dhidi ya Orlando Pirates - Ahmed Ali

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, ameendeleza kampeni ya kuhamasisha mashabiki wa klabu hiyo kuelekea mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates, utakaochezwa Jumapili katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Katika siku ya pili ya kampeni hiyo ya hamasa, Ahmed leo amekutana na Wanasimba wa Mbezi Makonde, ambako amesisitiza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu yao, akieleza kuwa ushindi katika mchezo huo unahitaji mshikamano wa kila Mwanasimba.

“Tusichukulie poa hii mechi, ni kweli sisi ni watemi, tunajua kucheza mechi za nyumbani, tuna timu bora, tuna mwalimu bora, tuna nafasi kubwa ya kupata ushindi, lakini hayo ya kupata alama tatu tutapata kama tukiwa na mshikamano wa kila Mwanasimba kila pembe ya dunia,” amesema Ahmed.

Alama tisa Uwanja wa Uhuru

Ahmed ameeleza kuwa malengo ya Simba ni kushinda michezo yote mitatu ya nyumbani katika hatua ya makundi na kukusanya alama tisa, huku akisisitiza kuwa safari hiyo inaanza kwa kuifunga Orlando Pirates Jumapili.

“Alama tisa katika Uwanja wa Uhuru ni kama damu na maji, huwezi kuvitenganisha. Tunataka kushinda mechi zote katika Uwanja wa Uhuru na alama hizo zinaanza kwa Orlando.”

Kufuzu robo fainali ni jukumu la kila Mwanasimba

Akizungumzia malengo ya klabu hiyo katika michuano ya msimu huu, Ahmed amesema bado wana machungu ya kuishia hatua ya makundi msimu uliopita, hivyo kila Mwanasimba anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha timu hiyo inafuzu hatua ya robo fainali.

“Jukumu la kuipeleka Simba robo fainali ni jukumu la kila Mwanasimba, sio kazi ya mtu mmoja, sio kazi ya Steve Barker peke yake, sio kazi ya viongozi peke yao, sio wachezaji peke yao na sisi mashabiki tuna kazi ya kuipeleka Simba robo fainali.”

Aidha, Ahmed amesema Simba inaiheshimu Orlando Pirates, lakini haina sababu ya kuiogopa kutokana na ubora na uwezo ilionao wa kushindana katika michuano ya kimataifa.

“Tunachohitaji sisi ni alama tatu na kila tukimtazama mpinzani wetu Orlando, kila tukimscan mpinzani wetu tunaona HUYU NI WETU. Tunamheshimu lakini tutaruka naye sambamba. Mnyama anataka alama tatu, Mnyama anataka ushindi wa kwanza. Tunaifikiria robo fainali, huu ni mwaka wetu Wanasimba.”

Simba yadhamiria kurejesha heshima yake kimataifa

Semaji huyo wa Wekundu wa Msimbazi amebainisha kuwa ajenda kuu ya Simba katika michuano ya kimataifa msimu huu ni kurejesha heshima yake na kufikia hatua za juu zaidi za mashindano.

“Agenda yetu kimataifa msimu huu ni moja, kurejesha heshima yetu. Tusikubali kila mwaka kushusha heshima yetu, ni muda sasa kuamka na kurudi kwenye levels ambazo hakuna timu yoyote ya Tanzania inaweza kufikia.”

Ahmed anaamini kuwa kufuzu hatua ya robo fainali kutafungua njia kwa Simba kupambana kuingia nusu fainali na hatimaye kufikia fainali ya michuano hiyo.

Wanasimba watakiwa kujaza Shamba la Bibi

Akihitimisha hamasa yake kwa Wanasimba wa Mbezi Makonde, Ahmed amewataka mashabiki kununua tiketi na kujitokeza kwa wingi Jumapili, akisisitiza kuwa uwepo wao uwanjani ni sehemu muhimu ya mafanikio ya timu.

“Unapokuja uwanjani wewe ni sehemu ya ushindi na ukitaka kubaki nyumbani wewe ni sehemu ya Simba kufeli. Siamini kama Mwanasimba huyo yupo, Tsh 7,000 unayo, usafiri unao na ukachagua kubaki nyumbani basi wewe ujue umechagua tubaki nyuma.”

Simba itaanza kampeni yake ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuikaribisha Orlando Pirates Jumapili, Novemba 29, 2026, katika Uwanja wa Uhuru, maarufu kama Shamba la Bibi, huku dhamira yake ikiwa ni kuvuna alama tatu muhimu na kuweka msingi imara wa kufuzu hatua ya robo fainali.

Simba SC Stories

Wagombea 40 wavuka mchujo wa awali Simba, Mangungu na Julio watemwa
Wagombea 40 wavuka mchujo wa awali Simba, Mangungu na Julio watemwa
21m ago
READ MORE →
Toure tayari kurejea dhidi ya Pirates
Toure tayari kurejea dhidi ya Pirates
8h ago
READ MORE →
Semaji awatisha Orlando Pirates 'watake, wasitake watapasuka'
Semaji awatisha Orlando Pirates 'watake, wasitake watapasuka'
8h ago
READ MORE →
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 27 2026
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 27 2026
12h ago
READ MORE →
Dozi ya Orlando Pirates inaandaliwa
Dozi ya Orlando Pirates inaandaliwa
23h ago
READ MORE →
Simba yazindua hamasa kuikabili Orlando Pirates, kaulimbiu ‘Huyu ni Wetu’
Simba yazindua hamasa kuikabili Orlando Pirates, kaulimbiu ‘Huyu ni Wetu’
1d ago
READ MORE →
Pirates wawasili Dar
Pirates wawasili Dar
1d ago
READ MORE →
Simba kuzindua hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Orlando Pirates leo
Simba kuzindua hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Orlando Pirates leo
1d ago
READ MORE →
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
1d ago
READ MORE →
Kuzishuhudia Simba vs Orlando Pirates kiingilio buku saba
Kuzishuhudia Simba vs Orlando Pirates kiingilio buku saba
2d ago
READ MORE →