Kiungo wa Simba, Neo Maema, amesema wachezaji wa timu hiyo wamejiwekea malengo ya kufanya vizuri katika mashindano yote wanayoshiriki msimu huu na wako tayari kupambania alama tatu katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates utakaochezwa kesho.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Maema amesema anatambua kuwa hautakuwa mchezo rahisi, lakini jukumu lao ni kuhakikisha wanaendeleza mwenendo mzuri walioanza nao msimu huu.
Maema amesema ana imani na uwezo wa kikosi chao wa kupata matokeo mazuri licha ya changamoto wanazotarajia kukutana nazo katika mchezo huo.
“Wachezaji wote tuliweka malengo ya kufanya vizuri msimu huu na hadi sasa tunashukuru tumeanza vyema. Tunahitaji kuendeleza mwendelezo huo katika mechi ya kesho na naamini tutaweza kupata ushindi licha ya ugumu wa mchezo huo,” alisema Maema.
Simba itaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira ya kuanza vyema kampeni yake ya hatua ya makundi kwa kusaka alama tatu muhimu dhidi ya Orlando Pirates.