Taasisi ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania (AKHST) imeingia makubaliano ya kutoa huduma za matibabu, mafunzo na uchunguzi wa afya kwa ujumla na klabu ya Azam kwa kipindi cha miaka miwili.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Februari Mosi, 2023 kwenye moja ya kumbi za mikutano za hospitali hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwahusisha Watendaji wakuu (CEO’s) wa taasisi zote mbili, Sisawo Konteh wa AKHST na Abdul Kareem ‘Popat’ wa Azam sambamba na viongozi wengine.
Mkataba huo unalenga kuimarisha uhusiano kati ya AKHST na Azam Fc, ukijikita zaidi kwenye kutoa huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vyote vya AKHST vilivyopo nchini ikiwemo upimaji wa afya, upatikanaji wa huduma za maabara na mionzi, mafunzo, ukarabati na huduma za uchunguzi, uhamasishaji wa habari za afya na elimu, na mashauriano zaidi ya kitaalamu kwa wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wanaotambulika wa klabu hiyo.