Mnyama ameunguruma dimba la Mkapa leo akiifumua Singida Big Stars mabao 3-1 katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira ameanza kujibu maswali ya Wanasimba kuhusiana na mbinu zake leo wakishuhudia kandanda safi kutoka kwa timu yao
Simba ilionyesha kuhitaji ushindi tangu dakika ya kwanza, na iliwachukua dakika nane tu kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Jean Baleke
Ikiwa ni mechi yake ya pili kwenye ligi, Baleke amefunga bao lake la pili, usajili bora unaoilipa Simba mapemaaa
Ilikuwa mpira wa adhabu kutoka kwa Chama uliotua kwenye guu la kushoto la Baleke na bila ajizi akaifungia Simba bao la kuongoza
Chama hakuwa amemaliza kutoa assist katika mchezo huo kwani dakika chache baadae akajaza mtungi mwingine kupitia mpira wa adhabu ambao safari hii ulijazwa kimiani na Saido Ntibazonkiza
Bao la 10 kwa Ntibazonkiza msimu huu, likiwa ni bao lake la sita tangu atue Simba
Bruno Gomez akaifungia Singida BS bao pekee kupitia mpira wa adhabu kabla ya timu hizo kwena mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-1
Kipindi cha pili Simba ilirejea na kasi ileile waliyomaliza nayo na hakuwa mwingine bali yule fundi wa mabao ya CAF, Pape Ousmane Sakho
Ilikuwa dakika ya 58 Sakho alifunga bao kama alilowafunga Asec Mimosas kwenye michuano ya CAF msimu uliopita na kushinda tuzo ya bao bora la CAF
Ni vilevile, safari hii akiitendea haki krosi ya Shomari Kapombe kutoka upande wa kulia
Ni alama tatu muhimu kwa Simba ambazo kwa hakika zimeendelea kuiweka Simba kwenye nafasi nzuri katika mbio za ubingwa