Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga leo wanashuka uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi huko Tunisia kumenyana na US Monastir
Ni mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ambao utapigwa saa 1 usiku
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri kunako uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi kwani ni katika uwanja huo walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Club Africain na kutinga hatua ya makundi
Katika mchezo huo Yanga inahitaji kushinda lakini hata matokeo ya sare yatakuwa muhimu sana kwa Wananchi
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema malengo yao katika michuano hiyo ni kutinga robo fainali hivyo leo wanahitaji kushinda au sare
Hersi alisema wana mkakati kabambe wa kuhakikisha wanashinda mechi zao tatu watakazocheza nyumbani na ugenini kuvuna angalau alama mbili
Kazi ya kusaka alama za ugenini wanaianza leo mbele ya Monastir ambayo imekuwa na msimu mzuri kwenye ligi ya Tunisia
Monastir ni vinara wa kundi A katika ligi ya Tunisia ambayo timu ziko katika makundi mawili
Lakini pia ikumbukwe Monastir ndio waliwaondosha mashindanoni mabingwa watetezi wa kombe la Shirikisho RS Berkane
Hivyo ni wazi utakuwa mchezo mgumu wenye upinzani mkali