Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika mkutano na Wanahabari, Nabi amesema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya US Monastir, wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo na sasa wako tayari kuikabili Mazembe
Nabi amewaomba radhi Mashabiki na Wanachama wa Yanga kutokana na matokeo hayo ambayo waliyapata baada ya kufanya makosa
"Tunawaomba radhi Mashabiki na Wanachama wetu kwa kupoteza mchezo dhidi ya Monastir. Yalikuwa makosa yetu lakini tumepata muda wa kufanyia kazi mapungufu yote na sasa tuko tayari kwa mchezo unaofuata dhidi ya TP Mazembe"
"Mashindano haya hayamaliziki kwa mechi moja hivyo bado tunayo nafasi ya kufanya vizuri katika mechi zote zinazofuata"
"Morali ya wachezaji iko juu, wanajituma mazoezini na kuonyesha wanataka kushinda mchezo dhidi ya TP Mazembe. Hali hiyo inanipa matumaini kuona tutakuwa na mchezo mzuri hapo kesho," alisema Nabib
Nabi amebainisha kuwa katika mchezo huo atawakosa wachezaji wawili Bernard Morrison ambaye ni majeruhi na Salum Abubakar 'Sure Boy' ambaye anauguliwa na mtoto
Aidha Nabi amesema kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki atafanyiwa tathmini baada ya mazoezi ya mwisho leo kuona utayari wake akiwa amekosa mazoezi kwa siku mbili kutokana na matatizo ya kifamilia
Nabi pia alijibu maswali ya wanahabari waliowaulizia wachezaji Mamadou Doumbia na Feisal Salum 'Fei Toto'
Nabi amesema Doumbia anaendelea kufanya mazoezi na wachezaji wenzake na sababu pekee inayomfanya hachezi kwa sasa ni kwa kuwa hana muunganiko na wenzake wakati suala la Feisal amesema sio kipaumbele kwa sasa kwa sababu kwa muda wote ambao amekosekana wachezaji wengine wametekeleza vyema majukumu yao
"Feisal ni mchezaji mzuri, tunafahamu bado ana mkataba na Yanga hivyo akirudi tutamkaribisha kwa mikono miwili lakini hata asiporudi sio kwamba Yanga haitaendelea"
"Wachezaji na makocha wanapita lakini Yanga itaendelea kubaki. Katika mwezi mmoja ambao amekosekana sisi benchi la ufundi tulitengeneza timu kwa kuzingatia wachezaji tulionao"
"Focus yetu kwa sasa ni mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao tunahitaji kushinda," alisema Nabi