Nyota chipukizi wa Ivory Coast, Sylla Moustapha amefariki baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu nchini humo kati ya klabu yake, Racing Club d’Abidjan na SOL FC kwenye Uwanja wa Robert Champroux jana.
Moustapha, anayecheza beki amefariki akiwa na umri wa miaka 21. Kupitia ukurasa wa Twitter , Racing Club imeandika
"Mlinzi wetu Sylla Moustapha amefariki jioni hii (Jumapili) baada ya kuugua akiwa uwanjani"
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe ametuma salamu za pole kwa familia ya Sylla Moustapha, Rais wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast Idriss Diallo, familia Racing Club d'Abidjan na watu wa Ivory Coast katika kipindi hiki cha majonzi
Huko Afrika Kusini klabu ya DStv Premiership, Richards Bay, jana ilitangaza kufariki kwa mmoja wa wachezaji wao waliocheza dhidi ya Kaizer Chiefs wikendi.
Kiungo wa kati wa klabu hiyo Siphamandla Mtolo, ambaye alikuwa na umri wa miaka 29, anaripotiwa kufariki dunia wakati wa mazoezi ya asubuhi ya klabu hiyo
"Ni kwa huzuni kubwa kutangaza kwamba Klabu ya Soka ya Richards Bay imempoteza mmoja wa viungo, Siphamandla 'Spepe' Mtolo. Alianguka leo asubuhi wakati wa mazoezi," ilisema taarifa ya klabu hiyo.