Kocha wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amewatoa hofu mabosi wa timu hiyo kwamba atainusuru timu isishuke daraja na msimu ujao itacheza Ligi Kuu
Polisi Tanzania leo Jumapili watashuka Uwanja wa Jamhuri kuwakabili Dodoma Jiji katika mchezo ambao utazikutanisha timu mbili zenye hali tete kwenye ligi
Polisi Tanzania ilimchukua Zahera mwezi Disemba 2022 baada ya kumtimua Joslin Sharif sambamba na msaidizi wake, Augustino Damian
Tangu Desemba 2, alipotangazwa kuwa kocha mkuu timu hiyo imecheza michezo 10 akishinda michezo miwili, ilipoichapa mabao 2-0 Namungo kisha ikaifunga Tanzania Prisons bao 1-0, sare nne na kuchapwa michezo minne.
Afisa Habari wa timu hiyo, Frank Lukwaro alisema Zahera amewahakikishia kupambana ili kukwepa kushuka daraja kwani wanashika nafasi ya 16 kwa alama 19
"Kitu kikubwa ambacho kocha alisema kuna tatizo eneo la ushambuliaji ambapo nafasi nyingi zilizokuwa zikipatikana zilikua hazizai matunda mazuri"
"Baada ya wiki mbili kukaa bila mchezo ameyafanyia kazi mapungufu hayo na kuahidi matokeo mazuri katika michezo inayofuata tukianza na Dodoma Jiji," alisema Lukwaro.
Lukwaro amesema hawajakata tamaa na matumaini ya kubaki Ligi Kuu ipo sababu michezo iliyobaki inaweza ikawafanya kupanda nafasi za juu kama watapata matokeo mazuri