Mshambuliaji wa Chelsea ambaye anaitumikia Inter Milan kwa mkopo, Romelu Lukaku jana alifunga hat-trick na kuiongoza Ubelgiji kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uswidi katika mechi ya kufuzu kwa Euro 2024
Yawezekana wengi wamepoteza imani kwa mshambuliaji huyu mwenye asili ya DR Congo, lakini anapokuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa, huwa ni tofauti
Ulikuwa ushindi muhimu kwa Ubelgiji waliopata ugenini katika mchezo ambao pia alishuhudiwa mshambuliaji mkongwe Zlatan Ibrahimovic akiterejea kuitumikia Sweden baada ya mwaka mmoja
Ibrahimovic, 41, aliingia dakika ya 73 kwa shangwe kutoka kwa mashabiki wa Uswidi. Ilikuwa ni mechi yake ya kwanza ya kimataifa baada ya kutangaza kustaafu mwaka uliopita.
Akiwa na umri wa miaka 41, miezi mitano na siku 21, Ibrahimovic alitajwa kuwa amevunja iliyokuwa ikishikiliwa na kipa wa Italia Dino Zoff tangu 1983, kama mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza mechi ya kufuzu michuano ya Ulaya.
Hata hivyo, mshambuliaji wa Gibraltar Lee Casciaro - ambaye ana umri wa siku nne zaidi ya Ibrahimovic - aliweka rekodi katika mechi ya timu yake kushindwa 3-0 nyumbani na Ugiriki katika Kundi B Ijumaa.
Wikiendi iliyopita, Ibrahimovic alikuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao katika historia ya Serie A wakati mshambuliaji huyo wa AC Milan alipofunga penalti dhidi ya Udinese.
Ibrahimovic amesema anataka kucheza Euro 2024 nchini Ujerumani mwaka ujao atakapofikisha umri wa miaka 42, na atakuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kushiriki michuano hiyo