Huku ikiwa na tiketi ya kucheza robo fainali mkononi, Simba imepanga kucheza kwa kiwango cha juu katika mechi yake ya kukamilisha ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Raja Casablanca itakayochezwa usiku wa leo kwenye Uwanja wa Mohammed V nchini Morocco
Kundi la pili la wachezaji wa timu hiyo limeshawasili Morocco tayari kwa mechi hiyo ambayo Wekundu wa Msimbazi wataitumia pia kama sehemu ya maandalizi ya hatua inayofuata ya mashindano hayo ya kimataifa.
Kocha Mkuu wa Simba, Robert Oliviera 'Robertinho' alisema kikosi chake sasa ni imara tofauti na kilivyokuwa wakati wanakutana katika mechi ya kwanza na Raja Casablanca.
Robertinho alisema pia yeye alikuwa na siku chache tangu alipojiunga na kikosi hicho, hivyo muunganiko wa timu ulikuwa bado haujakaa vyema.
"Tumeimarika idara zote, wanakutana na kikosi tofauti na kile cha mechi ya mkondo wa kwanza, wasitarajie mteremko, tunahitaji kushinda ili kumaliza kwa heshima, lakini tukionyesha ubora wetu," Robertinho alisema.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wamejiandaa vizuri na wamekwenda Morocco kwa ajili ya kulinda heshima ya klabu na taifa la Tanzania.
Rweyemamu alisema mechi hiyo haitakuwa rahisi kwa kila upande kwa sababu wenyeji wanataka kuendeleza ubora wao na Simba imejiimarisha kupindua meza.
Meneja huyo aliongeza hawatakubali kupoteza tena mechi hiyo ya marudiano na ndio sababu kubwa wamejiandaa kucheza kwa nguvu zote tofauti na baadhi ya wadau wanavyofikiri.
Alisema wamezungumza na wachezaji na kuwakumbusha hawataki kuingia katika rekodi mbaya kama ambayo ilivyotokea misimu iliyopita, hivyo watashuka dimbani kupambana kama vile bado hajawatinga hatua ya robo fainali.
"Kila kitu kimeenda sawa, kikosi cha pili kimewasili kwa ajili ya mechi ya mwisho. Tulipokwama Arusha kuna baadhi ya wachezaji walirejea Dar es Salaam na kesho yake wakaungana na wenzao waliobaki katika kikosi cha Taifa Stars wakaondoka nao, baada ya kufika Doha, Qatar wakakutana na wachezaji wengine ambao walikuwa wametoka kuzitumikia nchi zao, wakapanda ndege moja na kuwasili hapa, kwa hiyo kikosi kimekamilika"
"Kimsingi tumekuja katika mechi ya mashindano, kwa bahati mbaya tulipoteza mechi iliyopita kwa mabao 3-0, hivyo tumekuja huku kwa lengo moja kulinda heshima ya klabu na taifa kwa ujumla, hatutaki kuingia kwenye rekodi mbaya ya kupoteza, au kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao," alisema meneja huyo.
Aliongeza hawataidharau mechi hiyo kwa sababu bado wanaitumia kama njia ya kujenga timu kuelekea hatua inayofuata ya mashindano hayo.
Simba itashuka uwanjani katika mechi hiyo ikiwa kwenye nafasi ya pili na pointi tisa mkononi huku wenyeji wakiwa ni vinara wa kundi C baada ya kujikusanyia pointi 13 kibindoni.
Matokeo yoyote katika mechi hiyo hayatabadilisha msimamo wa kundi wakati Horoya ya Guinea na Vipers ya Uganda nao watakutana katika mechi nyingine ya mwisho ya kukamilisha ratiba.
Baada ya mechi hiyo kumalizia, Simba itarejea nchini kusubiri kufahamu mpinzani wake wa hatua ya robo fainali katika droo itakayochezeshwa Jumatano huko jijini Cairo, Misri.