Wanasema mfupa uliwashinda wengi umelika kilaini leo na Mnyama Simba!
Ni baada ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu Fc katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Highland Estates, Mbarali Mbeya
Kabla ya kipigo cha leo, Ihefu hawakuwa wamepoteza mchezo katika uwanja wao wa nyumbani dhidi ya timu kutoka jijini Dar es salaam
Yanga, KMC na Azam Fc zote zilichezea kichapo katika dimba la Ihefu
Hata hivyo mabao mawili ya mshambuliaji hatari wa Simba Jean Baleke yalitosha kuihakikishia alama tatu muhimu katika mchezo mgumu
Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake akiwaacha nje nyota wake muhimu
Mabadiliko hayo yaliibua lawama miongoni mwa mashabiki wa Simba kabla ya mchezo
Lakini Robertinho ameibuka shujaa baada ya dakika 90 timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0
Ni ushindi ambao unaifanya Simba iendelee kuweka hai matumaini katika mbio za ubingwa wakifikisha alama 60 alama tano nyuma ya vinara wa ligi Yanga wenye alama 65
Yanga itacheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Azam Complex siku ya Jumanne