Mlinda lango wa Rivers United ya nchini Nigeria, Victor Sochima ameweka wazi malengo yake msimu ujao ni kucheza timu kubwa hapa Tanzania huku akitaja miongoni mwao zinazomvutia ni matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC
Sochima alionyesha kiwango kizuri katika michezo yote miwili ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga hali iliyozifanya baadhi ya timu nchini kuanza mazungumzo naye ya kimya kimya
Sochima amesema timu nyingi zimefurahishwa na uwezo wake hivyo zilimfuata kuzungumza naye ingawa kwa sasa akili yake ameiwekeza kwa ajili ya kuhakikisha msimu huu unaisha
"Siwezi kuweka wazi kwenye kila kitu kinachoendelea lakini itoshe kusema ni kweli nimefuatwa na baadhi ya timu ikiwemo Yanga kwa sababu baada ya mechi yetu kuisha nilifuatwa na kocha wao, Nasreddine Nabi," alisema
Sochima aliongeza mbali na Yanga ila timu nyingine ambayo imeonyesha nia ya kuhitaji saini yake ni Azam ambayo kwake binafsi anatamani kuichezea kwani miundombinu iliyonayo inamshawishi tofauti na kwingine
"Pale Azam kuna rafiki yangu mkubwa anaitwa, Isah (Ndala) ni mchezaji mzuri ambaye nimekuwa naye kwa ukaribu hivyo nitafurahia kama itatokea siku moja tutacheza wote pamoja ingawa kwa sasa dili bado halijakamilika," alisema