Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba imewaomba radhi Wanachama na mashabiki wa timu hiyo baada ya kushindwa kufikia malengo msimu huu
Mwenyekiti wa Bodi Salim Abdallah 'Try Again' amesema hakuna anayepaswa kulaumiwa kutokana na kilichotokea msimu huu kwa kuwa kila mmoja alitimiza wajibu lakini ni bahati mbaya tu hawakupata matokeo waliyotarajia
"Tunawaomba radhi wanachama na mashabiki wetu baada ya kushindwa kufikia malengo yetu msimu huu, tutajipanga upya ili kuhakikisha msimu ujao tunafanya vizuri"
"Sidhani kama kuna yeyote anapaswa kulaumiwa kwa sababu sisi kama viongozi tulitimiza wajibu wetu, ni bahati mbaya tu matokeo tuliyoyatarajia hayakuwa"
"Tumefanya usajili mzuri kwa ushirikiano lakini baadhi ya wachezaji hawakufikia matarajio yetu, na hili ni kawaida hutokea. Sisi tuliwahi kumuuza Clatous Chama na Luis Miquissone wakiwa katika viwango vya juu kabisa lakini hawakufanya kile kilichotarajiwa katika timu zao mpya"
"Zipo sababu ambazo zinaweza kupelekea mchezaji asifanye vizuri, mfano kuzoea mazingira, hali ya hewa au majeruhi. Ismail Sawadogo alionyesha kiwango bora sana kwenye mchezo wake wa kwanza tulipomsajili lakini baadae akapata majeraha mwenyewe akalazimisha kutaka kuonyesha kile alichonacho matokeo yake haikuwa hivyo"
"Suala la majeruhi kwa baadhi ya wachezaji imekuwa changamoto pia, hila nadhani benchi la ufundi na madaktari wataweza kutueleza kitaam zaidi na nini kifanyike," alisema Try Again
Try Again amesema Simba ilishinda mataji karibu yote kwa misimu minne mfululizo, wapinzani wao nao walikuwa wakijipanga katika kipindi hicho na sasa wameimarika
Hivyo ni wakati wa Simba nayo kujipanga ili kuhakikisha msimu ujao inarejesha ubabe wake katika soka la Tanzania