Ushindi wa mabao 4-0 walioupata juzi Mashujaa FC dhidi ya timu kongwe ya Pamba FC ya Mwanza umeifanya timu hiyo ya Kigoma kusogelea kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao
Mashujaa sasa watalazimika kutafuta sare au ushindi wowote kwenye mchezo wa marudiano kuweza kucheza mchezo mwingine wa 'Play Off' dhidi ya mshindi wa mchezo kama huo kwa timu za Ligi Kuu zitakazoshika nafasi ya 13 na 14 kutafuta nafasi moja ya kubaki au kupanda Ligi Kuu.
Matokeo hayo ya juzi kwenye Uwanja wa Tanganyika mjini Kigoma hayakutarajiwa na wengi kutokana na ubora wa Pamba FC ambayo ilimaliza Ligi daraja la kwanza ikiwa kwenye nafasi ya tatu na pointi zake 59 ikizidiwa kwa pointi moja tu na Kitayose ya Tabora ambayo imepanda daraja moja kwa moja ikiungana na JKT Tanzania.
Katika mchezo huo wa juzi, Pamba ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi lakini wakakumbana na matokeo ya kushtukiza kwa kuambulia kipigo hicho.
Mechi ya marudiano kati ya timu hizo mbili itachezwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Timu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu nazo zitacheza mechi ya mchujo 'play off' kupata timu itakayocheza na Mashujaa FC.
Awali ratiba ya Bodi ya Ligi ilionyesha timu hizo zingecheza Jumapili ijayo na Juni 3, lakini kutokana na ratiba ya ligi kusogezwa mbele ili kupisha mechi za fainali za wawakilishi wa Tanzania, Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger, Mei 28 na Juni 3, mechi hizo zimeahirishwa kwani ligi itakuwa bado haijamalizika.



