Kocha wa Simba, Robert Oliveira 'Robertinho', amesem anataka ashirikishwe katika kila hatua ya usajili watakaofanya kuelekea msimu ujao baada ya kukabidhi faili la majina ya wachezaji anaowataka kwenye kikosi chake
Kocha huyo raia wa Brazil amesema ili kupata wachezaji ambao wanakidhi mahitaji yake, anataka ashirikishwe kwenye kila hatua ya usajili
Msimu huu haukuwa mzuri kwa Simba baada ya kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu
Simba walikuwa na malengo ya angalau kucheza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kombe la Shirikisho (FA), hata hivyo wameshindwa kufikia malengo hayo na kushuhudia watani zao, Yanga wakichukua ubingwa wa Ligi Kuu na kutinga hatua ya fainali katika michuano ya Shirikisho Afrika na ile ya FA.
"Nashukuru Mungu kwa sasa tunasubiria kumaliza msimu kwa mechi mbili zilizobakia kabla ya kuanza maandalizi ya msimu ujao, ingawa tumeanza mikakati mapema ya kujua mahitaji gani ambayo tunaweza kuyahitaji kuelekea msimu ujao kwa sababu msimu huu hakuna ambacho tumeweza kukipata"
"Kuhusu suala la usajili tayari tumeanza mikakati kwa sababu tunaelewa tumekosea wapi na kitu gani tunapaswa kufanya ili tuweze kuwa bora msimu ujao hivyo ni jambo jema kuweza kutambua kila hatua ya usajili wa wachezaji ambao tumelenga kuwasajili kupitia viongozi na ripoti itakavyoweza kuonyesha mahitaji yetu ya msimu ujao, " alisema Robertinho
Alisema kwa sasa wanaangalia michezo miwili iliyobakia na amewataka wachezaji wake kupambana kushinda mechi mbili zilizosalia ili kumaliza ligi hiyo kwa heshima.
Wachezaji wa Simba walipewa mapumziko baada ya mechi za kuhitimisha msimu kusogezwa mbele hadi Juni 06 na Juni 09 wakitarajiwa kurejea mazoezini May 24