Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira amewapongeza wachezaji, viongozi wa Simba na mashabiki kwa umoja na ushirikiano ambao umepelekea wakashinda taji la kwanza msimu huu
Simba imetwaa Ngao ya Jamii baada ya ushindi wa mikwaju ya penati 3-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali uliopigwa jana katika uwanja wa Mkwakwani
Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana, hivyo mshindi kuamuliwa kwa changamoto ya penalti
Mlinda lango wa Simba Ali Salim alikuwa shujaa katika mchezo huo akiokoa penalti tatu
"Nafurahi tumetimiza malengo yetu. Tulitarajia mchezo utakuwa mgumu kwa sababu hakuna mechi ya derby rahisi, lakini sisi tuliingia na mkakati wetu ambao wachezaji waliukamilisha"
"Nafikiri tulicheza vizuri kwenye kipindi cha kwanza tukiwa na mpira na hata bila ya mpira. Kipindi cha pili tulifanya mabadiliko ya uchezaji na baadhi ya wachezaji ili kuongeza presha katika lango la wapinzani"
"Nawapongeza wachezaji wangu, nampongeza kipa wetu (Ally Salim) ni kijana mdogo lakini tangu msimu uliopita kwenye ligi ya mabingwa amekuwa mchezaji muhimu kwetu"
"Nampongeza kila mmoja, sote tumeshirikiana kupata mafanikio haya, tumeshinda taji la kwanza msimu huu," alisema Robertinho
Salim anastahili tuzo ya nyota wa mchezo huo jana lakini pia pengine ndiye mchezaji bora wa michuano ya Ngao ya Jamii kwani hata katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida FG, alidaka mkwaju wa penati na kuisaidia Simba kutinga fainali
Kwa hakika Salim ameonyesha ukomavu na pengine ataleta ushinda katika eneo la golikipa ambalo juzi Simba ilimuongeza Ayoub Lakred kutoka Morocco