Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amefanya kazi katika viwanja vya mazoezi kuhakikisha eneo la ushambuliaji linatumia vyema nafasi zinazotengenezwa
Yanga ilikuwa bora katika michuano ya Ngao ya Jamii iliyofanyika wiki iliyopita mkoani Tanga, lakini Wananchi walishindwa kutetea Ngao hiyo baada ya kushindwa kufunga bao katika dakika 90 za mchezo wa fainali dhidi ya Simba na kupoteza kwenye mikwaju ya penati
Baada ya kurejea Dar es salaam, kabla ya kuanza maandalizi ya mchezo wa awali ligi ya mabingwa dhidi ya Asas Fc, Gamondi alifanya kikao na washambuliaji wake
Mtihani wa kwanza kwa washambuliaji Hafiz Konkoni, Kennedy Musonda na Clement Mzize ni Jumapili katika mchezo dhidi ya Asas Fc
Hesabu za Gamondi ni kuona washambuliaji wanakuwa watulivu na kutumia nafasi kufunga mabao
"Tunacheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, ila bado tunapoteza utulivu kidogo kumalizia kule mbele, ni jambo zuri tumeliona hili mapema, hivyo tunalifanyia kazi"
"Tunahitaji kuboresha kitu na hili sio la mtu mmoja ni kati ya makocha na washambuliaji, tunaamini kutakuwa na mabadiliko taratibu," alisema Gamondi