Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Mpia Nzegeli ameweka wazi kuwa malengo yake ni kuhakikisha kuwa anaisaidia timu hiyo kufanya vyema katika michuano ya kimataifa na kufikia malengo yao ya kufika hatua ya makundi
Yanga ili wafanikiwe kutinga katika hatua ya makundi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanawaondoa Al Merrikh katka mchezo unaofuata wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Maxi amesema kuwa malengo yake ni kuhakikisha anaisaidia Yanga kufika kwenye malengo kwenye michuano hiyo kwa kufika katika hatua ya makundi huku akiamini kuwa wana uwezo mkubwa wa kuwaondoa Al Merrikh
"Malengo ya timu ndio malengo ya wachezaji wote, kwetu sisi tunatamani kuona tukifika katika makundi na kupita zaidi ya hapo, kikubwa kwetu tunachokifanya kwa sasa ni kuona tunajikita zaidi katika kufanya vyema katika michezo yetu"
"Michezo yetu miwili iliyopo mbeleni dhidi ya Al Merrikh ni muhimu zaidi kwa upande wetu kuona tunafanya vyema na kupata matokeo, tunaamini tunao uwezo huo na tutapambana zaidi kufikia hayo malengo," alisema
Maxi amekuwa na mwanzo mzuri katika kikosi cha Yanga akifunga mabao mawili, kutoa pasi moja ya bao kwenye mechi ya hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Asas Fc
Maxi pia amefunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao katika mechi mbili alizocheza kwenye ligi kuu ya NBC