Mlinzi wa kati wa Azam Fc, Abdallah Kheri 'Sebo', atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti lake la mguu wa kulia
Sebo ameumiza gegedu 'cartilage' ya maungio ya goti lake la mguu wa kulia, ambayo imelika na pia ameumiza mifupa midogo midogo kutokana na mlalo wa goti lake la kulia na tege alilokuwa nalo
Beki huyo kisiki, amefanyiwa upasuaji huo leo Jumatatu asubuhi, kwenye Hospitali ya Vincent Palloti, jijini Cape Town, Afrika Kusini
Sebo alipata majeraha hayo kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons, ambao Azam Fc ilishinda mabao 3-1, ambapo alilazimika kutolewa wakati wa mapumziko, nafasi yake ikichukuliwa na Nathan Chilambo
Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliambatana na beki huyo, amesema kuwa Sebo atarejea kwenye soka la ushindani baada ya miezi mitatu ya matibabu ya majeraha yake kumalizika
"Sebo amefanyiwa upasuaji wa kisasa unaoitwa arthroscopic, ambao wametoa mifupa midogo midogo iliyokuwa imevunjika na kupandikiza gegedu nyingine. "Baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mchezaji ameelekezwa mazoezi ya kufanya kwa muda wa mwezi mzima na anatakiwa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu," alisema Dr. Mwankemwa