Ugeni wa viongozi wa soka wapatao 250 kutoka maeneo tofauti duniani unatarajiwa kuanza kuingia leo Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki tukio la uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Mpira wa Miguu Afrika (AFL) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 20 litakalohusisha mechi baina ya Simba na Al Ahly
Msafara huo unaoongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe utahusisha wakuu wa idara mbalimbali za mashirikisho hayo, maraisi wa vyama na mashirikisho ya soka kwa nchi zote Afrika pamoja na marais waalikwa wa mashirikisho ya mabara mengine
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay alisema Tanzania ipo tayari kuupokea ugeni huo mkubwa ambao utashiriki sherehe za uzinduzi huo
"Marais wote wa vyama na mashirikisho ya soka Afrika watakuwepo, sekretarieti ya CAF itakuwepo. Maofisa wakubwa wa FIFA watakuwepo hapa hivyo ni msafara wa zaidi ya watu 200 utakuwepo hapa wameshaombewa vibali. Kwa hiyo serikali imeshafanya maombi katika hoteli zote kubwa na zimeshajaa"
"Tunategemea kuwa na shughuli kubwa sana ambayo imebeba watu wakubwa katika mpira wa miguu duniani hivyo ni faraja na fahari kwa taifa kupokea ujumbe mkubwa kama huo," alisema Ally Mayay
Mayay alisema kuwa maandalizi ya msingi kwa ajili ya kupokea ugeni huo na uzinduzi wenyewe ya mashindano hayo kwa asilimia kubwa yamekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni ujio wa viongozi hao pamoja na tukio lenyewe



