Jumapili ya wiki hii nyasi za uwanja wa Azam Complex zitawaka moto pale mabingwa wa ligi kuu ya NBC Yanga watakaposhuka uwanjani kuikabili Azam Fc katika mchezo wa ligi
Ni mchezo ambao Yanga itakuwa mwenyeji, Yanga ilichagua kucheza mechi zake za nyumbani hapo Azam Complex baada ya uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kwa ajili ya ukarabati
Awamu ya kwanza ya ukarabati uwanja wa Mkapa imekamilika lakini uwanja huo utafunguliwa kwa ajili ya mechi za AFL na mchezo dhidi ya Simba utakaopigwa Novemba 05 ambapo baada ya mchezo huo uwanja utafungwa tena kwa ajili ya awamu ya pili ya ukarabati
Habari njema kwa Yanga ni kuwa wachezaji wameuzoea uwanja wa Azam Complex kwani mechi zote tatu za nyumbani kwenye ligi kuu na mechi nyingine tatu kwenye ligi ya mabingwa zote zilipigwa Azam Complex
Yanga ina rekodi ya aina yake katika mechi ilizocheza dimba la Azam Complex, mara ya mwisho kupoteza mchezo kwenye uwanja huo ilikuwa Januari 2020
Aidha Wananchi hawajapoteza mchezo wowote dhidi ya Azam Fc katika mechi sita zilizopita, ushindi ni mechi tano na sare ni mechi moja
Sare pekee waliyopata Azam Fc ni msimu uliopita kwenye ligi kuu ya NBC. Mara ya mwisho kwa Azam Fc kupata ushindi dhidi ya Yanga ni April 25 2021 ukiwa ni mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Kabla ya kuanza msimu huu, Yanga na Azam Fc zilikutana kwenye Ngao ya Jamii mkoani Tanga Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0