Wakati ikiwa imesalia wiki moja kabla ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Asec Mimosas, bado uongozi wa Simba haujamtangaza kocha mpya atakayerithi mikoba ya Robertinho Oliveira
Ni wazi kwa muda uliobaki kuelekea mchezo huo Kaimu Kocha Mkuu Daniel Cadena na Kocha Msaidizi Seleman Matola huenda wakapewa jukumu la kuikabili Asec
Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ally amesema mchakato uko kwenye hatua za mwisho lakini kuna mambo machache yanawekwa sawa kabla ya kocha huyo kutangazwa
"Mchakato umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80, kuna mambo machache yanawekwa sawa kabla ya kocha kutangazwa. Uongozi umekuwa makini wakati huu ili kuhakikisha tunapata kocha ambaye ataendana na mipango na malengo yetu," alisema Ahmed
Mkufunzi wa zamani wa USM Alger Abdelhak Benchikha ndiye aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutua Msimbazi lakini inaelezwa mahitaji ya kocha huyo ni makubwa, Simba italazimika 'kuvunja benki' ili kumudu gharama zake
Benchikha aliiongoza USM Alger kushinda taji la Shirikisho msimu uliopita na mwanzoni wa msimu huu akashinda Super Cup akiifunga Al Ahly
Yuko kwenye tuzo za CAF, akiwania tuzo ya kocha bora wa mwaka, ana nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo