Mtendaji Mkuu wa Simba Imani Kajula amesema kocha Abdelhak Benchikha amepewa mkataba wa miaka miwili kuwanoa wekundu hao wa Msimbazi
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Kajula amesema haikuwa rahisi kumpata kocha huyo lakini ilikuwa dhamira ya uongozi wa Simba kumleta kocha ambaye ataifikisha klabu mbali
"Leo tunatamatisha shauku iliyokuwepo kwa siku kadhaa. Haikuwa jambo rahisi maana lengo letu kama klabu tulitaka mwalimu ambaye atatupeleka mbali. Kumpata mwalimu mzuri ni mchakato mkubwa sana"
"Mwalimu Benchikha atakuwepo kwa mkataba wa misimu miwili. Bodi ya Simba, menejimenti ya Simba imempa mwalimu uhuru wa kufanya kazi. Sisi ni moja ya klabu bora Afrika hatuwezi kufanya kazi kwa kumbana"
"Walimu ambao kocha Benchikha amekuja nao ndio aliochukua nao ubingwa wa Shirikisho Afrika na Super Cup. Kocha Farid amefanya kazi na Benchikha kwa miaka 30 pamoja na kocha Kamal amefanya nae kazi kwa karibu," alisema Kajula
Naye Benchikha amesema kujiunga na Simba ni jambo alilokuwa akilisubiri kwa hamu. Benchikha amesema tayari anafahamu mambo mengi kuhusu Simba hivyo amekuja kuhakikisha anarejesha furaha ya Wanasimba
"Nina furaha kubwa kuwepo hapa. Tangu nilipoanza kuwasiliana na viongozi nilikuwa na shauku ya kuja. Jambo kubwa ambalo naomba ni mashabiki kutupa ushirikiano na naamini kupitia hilo tutafanikiwa pamoja."
"Kuna mambo mengi ambayo tayari nayajua na nimekuja na mikakati ambayo nitaifanyia kazi. Kuhusu wachezaji tutajua zaidi nikishaanza kazi, kuhusu mashindano ya ndani na kimataifa yote ni muhimu. Mimi ni mpambanaji na nitapambana hadi tutafika"
"Mafanikio yatajengwa na Wanasimba wote hilo ndio muhimu zaidi. Kwa wachezaji sitaangalia majina bali anayefanya vizuri, kiwango cha mchezaji ndio kitafanya nimtumie," alisema Benchikha