Baada ya kupoteza alama mbili mkoani Kagera, leo Yanga ina mtihani mwingine mbele ya Dodoma Jiji katika mchezo wa ligi kuu ya NBC ambao utapigwa uwanja wa Azam Complex
Ni mtihani kwa sababu Dodoma Jiji hajawahi kuwa mpinzani mwepesi kwa Yanga licha ya Wananchi kuwa na matokeo mazuri dhidi yao
Mara ya mwisho timu hizo kukutana dimba la Azam Complex ni msimu uliopita ambapo Yanga ililazimika kutokea nyuma na kuibuka na ushindi wa jiooooni wa mabao 4-2 ambao uliwahakikishia Wananchi ubingwa wa 29 Ligi Kuu ya NBC
Wakati huu Dodoma Jiji wanakuja kuchuana na Yanga wakiwa na kocha mpya, Francis Baraza aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar na Biashara United kabla ya kurejea kwao Kenya
Mkufunzi wa Yanga Miguel Gamondi anafahamu leo wanazihitaji alama zote tatu ili kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi
Matokeo tofauti na ushindi yanaweza kupelekea presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ambao hawakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yao katika mchezo uliopita
Mchezo huo utapigwa kuanzia saa 1 usiku



