Yanga yachukua hatua kumalizana na Kambole

Joel JJ By Joel JJ β€’ 1st May 2024


Yanga yachukua hatua kumalizana na Kambole

Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema uongozi umechukua hatua kumaliza changamoto zinazopelekea wakumbane na rungu la kufungiwa kusajili na FIFA mara kwa mara

Jana Yanga ilipokea taarifa ya kufungiwa kutokana na madai ya aliyekuwa mchezaji wao Lazarus Kambole ambapo Yanga ilipaswa kukamilisha malipo ya mchezaji huyo ndani ya siku 45

Kamwe amesema tayari Yanga ilishaanza kumlipa mchezaji huyo kwa awamu lakini walichelewa kuwasilisha malipo ya awamu ya mwisho

"Taarifa ya kweli na tayari uongozi wetu umeshachukua hatua za kulimaliza Jambo hili. Ni fedha za awamu ya mwisho ambazo kwa mujibu wa makubaliano, tunapaswa kuzilipa kama ambavyo tulishalipa awamu zilizopita kwa mchezaji Kambole," aliandika Kamwe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii

Aidha Kamwe amewataka Wanachama na Mashabiki wa Yanga kujiunga/kulipia kadi zao za uanachama ili kuhakikisha timu inaepuka kadhia za aina hii zinazojirudia kila mara

"Kama na wewe ni sehemu ya watu walioguswa na Taarifa hii na mpaka sasa Hujalipia kadi yako ya Uwanachama, basi tambua wewe ndio unashiriki kwa asilimia kubwa kuirudisha nyuma klabu yako"

"Muda huu tunapoketi kwenye vijiwe vya soka na kujivunia/kutamba kuhusu ubora wa klabu yetu ni lazima tutambue kuna kazi kubwa inafanyika kuiweka Yanga yetu kwenye levo hizo"

"Viongozi wanaumiza sana vichwa kuhakikisha wanabuni vyanzo mbalimbali vya kuongeza pato la klabu yetu na kumsaidia bosi wetu GSM katika kuipeleka klabu yetu kwenye nchi ya ahadi"

"Niwaombe, tuwasaidie viongozi wetu. Sisi Wanachama Jukumu letu kubwa kwa sasa ni KULIPA ADA zetu kila Mwaka. Hili ni MUHIMU mno na ddio linapaswa kutuumiza mno pale unapomuona Mwananchi mwenzako akiwa anavimba na Yanga na hajalipia ada yake ya Uwanachama"


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.