Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ali amewataka mashabiki wa timu hiyo mkoani Arusha kujitokeza kwa wingi uwanja wa Sheikh Amri Abeid siku ya Jumamosi, May 25 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC
Akizungumza katika tawi la Wanasimba la Arusha Terminal mapema leo, Ahmed alisema wameupeleka mchezo huo Arusha kwa kutambua wingi wa Wanasimba katika mkoa huo akiamini watakwenda kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao katika mchezo ambao wanahitaji ushindi mnono ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao
"Kikubwa kilichotuleta Arusha ni mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC, mchezo ambao utachezwa tarehe 25 majira ya saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Tangu nimekuwa msemaji wa timu yenu timu haijawahi kuja Arusha hivyo nikaona hii ni nafasi nzuri ya kuja tuonane. Nimefurahi kwa mapokezi mazuri na hii inaonyesha Wanasimba wana imani na timu yao. Tumeileta mechi Arusha kwa kutambua thamani na mchango wa Wanaarusha kuipambania timu yao"
"Mechi ilikuwa imeshapangiwa uwanja, na kutoka uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kambini kwetu ni dakika mbili lakini tukasema tuipeleke Arusha wakaione timu yao. Mara ya mwisho Arusha kuiona Simba ilikuwa ni Novemba 22, 2020 tulicheza na Coastal Union na kuwafunga bao 7-0."
"Tumewaletea Wanasimba timu yao wafurahie kuiona. Sababu nyingine ni umuhimu wa mchezo wenyewe, wote mnafahamu tupo kwenye vita kubwa ya kupambania kwenda Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Mechi ngumu kama hizi lazima upeleke kwa watu wagumu wagumu, baada ya tathmini watu wagumu wanapatikana wapi, tukasema tupeleke Arusha"
"Wanasimba wa Arusha ni watu wa kipekee, nusu na robo ya mkoa huu ni mashabiki wa Simba. Kwahiyo tumekuja nyumbani, tunaamini hapa nyumbani Arusha tutapata tunachokitaka. Mnyama kwa mapenzi yake Mungu na juhudi za Wanaarusha, Mnyama anakwenda kutakata Mei 25. Kuleta timu hapa sio jambo la bahati mbaya hivyo mna kazi kubwa ya kuhakikisha Simba inakwenda Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Msimu ujao tunahitaji kuongeza alama za CAF, na njia pekee ni kushikiri Ligi ya Mabingwa Afrika sababu ndio michuano yenye pointi nyingi" alisema Ahmed
Ahmed ametangaza viingilio vya mchezo huo utakaopigwa saa 10 jioni ambapo Mzunguko - Tsh. 10,000, VIP C - Tsh. 15,000 na VIP A - Tsh. 30,000
Kikosi kitawasili Arusha Ijumaa majira ya saa 12:40 alfajiri na baadae kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Tiketi zinaanza kuuzwa leo



