Wakati ikianza kutangaza majina ya wachezaji inayowaacha, Coastal Union iko mbioni kumsajili winga wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda, lengo ikiwa ni kujiimarisha kuelekea mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, imefahamika
Habari kutoka ndani ya Coastal Union zinasema mazungumzo na Kisinda yameshaanza, na endapo yakienda vyema, basi mchezaji huyo atamwaga wino katika klabu hiyo
"Tunaendelea na usajili, na tunalenga wachezaji ambao ni wazoefu kwenye michuano ya kimataifa, huwezi kwenda kucheza huku ukiwa na vijana wengi, wakongwe, siyo wa umri, ila kwenye mechi kubwa wanahitajika, hivyo tunamkata Kisinda, najua atakuja kutusaidia kwa sababu amecheza klabu kubwa kama AS Vita, Yanga na RS Berkane," kilisema chanzo
Siku chache kabla ya taarifa hizi, Ofisa Habari ya Klabu hiyo, Abbas El Sabri, alikiri kufanya mazungumzo ya mchezaji mwingine raia ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Djuma Shaaban
"Ni kweli tupo katika mazungumzo na Djuma, ni mchezaji mzuri, mzoefu katika mechi za kimataifa. Unajua tangu tulipopata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho, tayari kama klabu tukatambua mahitaji yetu yataongezeka, kuanzia gharama, wachezaji na hata muda utakuwa finyu," alisema El Sabri
Mbali na huyo ambaye Coastal Union imekiri, lakini taarifa zinasema wanaendelea na mazungumzo na Saido Ntibazonkiza aliyeachwa na Simba hivi karibuni