Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids amesema maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahli Tripoli yamekamilika akiwa na matumaini makubwa ya kushinda mchezo huo na hatimaye kufuzu hatua ya makundi CAF CC
Fadlu amesema watakwenda katika mchezo huo wakiwa na mpango mkakati tofauti na ule waliotumia walipokuwa ugenini
"Tulicheza mechi ya kwanza ugenini tukiwa na lengo la kutoruhusu bao na pia kutafuta angalau bao la ugenini"
"Tulifanikiwa mpango wa kwanza wa kutoruhusu bao lakini hatukufanikiwa mpango wa pili wa kufunga bao ugenini"
"Kesho tuko nyumbani lakini tutahitaji kuwa makini ili kuhakikisha haturuhusu wao kufunga bao la ugenini kwani wakifunga bao moja sisi tutalazimika kufunga mawili"
"Hii haimaanishi kwamba tutacheza kama tulivyokuwa ugenini, tutabadilika, tutacheza kwa kushambulia na kuchukua tahadhari katika ulinzi pia"
"Wapinzani wetu bado hawafahamu ni mfumo gani tutatumia katika mchezo huu wa pili hilo ni jambo la faida kwetu, kile walichokishuhudia Libya sio watakachokiona kesho," alisema
Fadlu pia amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa kuwapa hamasa wachezaji wao
"Tunawahitaji mashabiki wa Simba waje kwa wingi uwanjani, naamini wingi wao utatuongezea ari na morali ya kupambana na kufanikisha malengo yetu ya kushinda mchezo"