Uwepo wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), kumetajwa kuwa kutaathiri moja kwa moja ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, alisema mabadiliko ya ratiba za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwenye michuano ya CHAN na Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, moja kwa moja yataathiri ratiba hiyo, hivyo watakaa na kufanya marekebisho
"Tunaendela kufanya marekebisho na maboresho ya ratiba baada ya Kamati ya Utendaji ya CHAN kukaa na kufanya marekebisho ya ratiba zao. Fainali ya CHAN zimepangwa kufanyika hapa Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi mpaka 28, lakini pia kuna mechi za 'play off' za kwenda kucheza hizo fainali ambazo zitaanza Oktoba 25 hadi 27, maana yake wamekuja kuathiri ratiba yetu moja kwa moja," alisema Kasongo
Alisema pia kutokana na hayo, ni lazima wafanye marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ili kuruhusu wachezaji watumikie timu yao ya taifa. Mbali na hilo, Kasongo pia alisema CAF imebadilisha pia ratiba za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambalo kwa kawaida lilitakiwa lichezwe mwezi Oktoba, sasa linararajiwa kuanza Novemba hadi Januari hivyo kuathiri pia Kombe la Mapinduzi ambalo hufanyika Januari Mosi hadi 13 mwakani
"Januari kuna Kombe la Mapinduzi, lakini kwenye ratiba ya CAF kutakuwa na michezo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho timu za Simba na Yanga zikiwapo. Ikumbukwe Simba na Yanga kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kipindi hicho watakuwa kwenye mechi za makundi, ingawa kwa hili sitaki sana kuelezea, kamati yenyewe ipo na klabu zipo zinaweza kulisemea, ila kwetu sisi tutalazimika kufanya marekebisho ya ratiba kutokana na kalenda hiyo ya CAF, kupisha CHAN na mechi za kimataifa," alisema Kasongo