Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ali amesema timu hiyo imejipanga kufanya vizuri katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika msimu huu ambapo watahakikisha wanachukua alama tatu katika kila mchezo utakaochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Jumatano, Novemba 27 Simba itaikaribisha Bravos ya Angola katika mchezo wa kwanza wa kundi A ambalo linaundwa na timu za Simba, CS Consstantine, CS Sfaxien na Bravos
Akizungumza katika matukio ya kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao, Ahmed alisema mkakati wao ni kuvuka hatua ya robo fainali na hivyo ni lazima washinde kila mchezo nyumbani
"Tarehe 27 tuna jambo kubwa kwenye Uwanja wa Mkapa. Tunahitaji kuanza vizuri hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ushindi wa Simba unakutegemea wewe Mwanasimba, tambua ya kwamba tiketi utakayonunua ni silaha muhimu ya kuisaidia Simba siku hiyo"
"Tunatambua siku hiyo ni siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ukishamaliza kupiga kura yako elekea Uwanja wa Mkapa. Asibaki Mwanasimba siku hiyo, tambua kwamba ushindi wa Simba unapatikana kwa ushirikiano wa nguvu wa kila Mwanasimba"
"Tumejiandaa siku hiyo kila Mwanasimba atakayekuja uwanjani aondoke na furaha. Tumedhamiria msimu huu kila anayekuja lazima tumefunge. Kwahiyo ndugu zangu Wanasimba jukumu letu la msingi ni kwenda uwanjani na ukienda uwanjani usitulie, unafanya balaa unaloweza," alitamba Ahmed
Aidha Ahmed amejitanga kuwa yeye ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo utakaopigwa Jumatano kuanzia saa 10 jioni
