Nyota Simba wanaitaka mechi dhidi ya CS Constantine

Joel JJ By Joel JJ
β€’
3 Dec 2024
Nyota Simba wanaitaka mechi dhidi ya CS Constantine

Nyota wa Simba, wameapa kupigana kufa kupona ili kupata ushindi au hata sare kwenye mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho, hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine ya Algeria, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids akisisitiza ni ushindi tu

Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka keshokutwa, Jumatano kwenda kwenye mji wa Constantine kucheza mechi hiyo ya Kundi A, dhidi ya timu hiyo utakaopigwa, Jumapili saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Mohamed Hamlaoui

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mchezaji mkongwe wa timu hiyo, Mzamiru Yassin, alisema wao kama wachezaji wako kwenye mazoezi makali kwa ajili ya maandalizi kwani wanatambua hautakuwa mchezo rahisi kama wengi wanavyodhani, lakini dhamira yao ni kwenda kusaka pointi katika mchezo huo

"Mechi ni ngumu, si nyepesi kama watu wanavyofikiria, sisi wengine ni wazoefu kwenye michuano hii, tunajua hilo, kinachotuaminisha hivyo ni kwamba mpinzani wetu tunaekwenda kucheza naye ametoka kushinda ugenini, akiifunga timu kubwa kama CS Sfaxien ya Tunisia ambayo kwenye kundi letu ndiyo ina historia nzuri ya michuano hii kuliko timu yoyote"

"Kama hao jamaa Watunisia wamefungwa kwao, ina maana si timu ya kubeza, ndiyo maana tumekomaa kwenye mazoezi," alisema mchezaji huyo aliyejiunga na timu hiyo mwaka 2016, akitokea Mtibwa Sugar

CS Sfaxien, imetwaa Kombe la Shirikisho Afrika mara tatu, mwaka 2007, 2008 na 2013. Alisema wachezaji wa Simba wanatambua kuwa wapinzani wao watataka kushinda mchezo huo ili waongeze matumaini ya kusonga mbele baada ya kushinda ugenini, hivyo hawatokubali kuona hilo likitokea

"Ni mechi ambayo wapinzani wetu wataichukulia umuhimu sana kwani wameshashinda ugenini, watataka kushinda kwao ili wawe kwenye nafasi nzuri ya kufuzu makundi, wachezaji tunajua hilo, ndiyo maana tumejiandaa kwenda kuchukua pointi tatu, ikishindikana moja kwani tayari tumeshachukua tatu nyumbani dhidi ya Bravo do Maquis, nao pia watakuja nyumbani,", alisema mchezaji huyo anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji

Alilisifia benchi la ufundi la timu hiyo, likiongozwa na Fadlu Davids kuwa linafanya kazi kubwa na akikiri kwa miaka ya karibuni hajaona benchi bora kama hilo

"Nafasi ya kusonga mbele hatua ya robo fainali tunayo, ila haitoki mdomoni, bali kwa jitihada, lakini naamini tutapita kwani safari hii tuna benchi la ufundi zuri sana," alisema

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu, amesema ushindi siku zote si zawadi bali ni kushindana, akisema huwezi kwenda uwanjani ukatarajia kushinda kama hujaandaa vizuri kikosi kwenye uwanja wa mazoezi

"Tunaitengeneza timu ili kwenda kushinda mechi, malengo ya klabu ni kufika hatua ya robo fainali, lakini hauwezi kufika kama hushindi mchezo. Tunakwenda kucheza na CS Constantine, nadhani inaweza kuwa ni timu ngumu zaidi kwenye kundi hili, inacheza vizuri, ina kikosi kizuri, lakini tutakwenda kupambana," alisema Fadlu

IPP Media

ADVERTISE HERE

More Stories

De Klassiker hakuna mshindi, Bayern 2-2 Dortmund
De Klassiker hakuna mshindi, Bayern 2-2 Dortmund
1h ago
READ MORE β†’
Natumaini Caf itaidhinisha uhuru stadium kwa mechi za makundi : Wallace Karia
Natumaini Caf itaidhinisha uhuru stadium kwa mechi za makundi : Wallace Karia
3h ago
READ MORE β†’
Azam FC yaibuka na ushindi ugenini dhidi ya JKT Tanzania
Azam FC yaibuka na ushindi ugenini dhidi ya JKT Tanzania
3h ago
READ MORE β†’
Brighton yaizamisha Manchester City Etihad, mbio za ubingwa zazidi kupamba moto
Brighton yaizamisha Manchester City Etihad, mbio za ubingwa zazidi kupamba moto
4h ago
READ MORE β†’
Orlando Pirates yawasha moto kwenye dabi ya Soweto, Simba yapata onyo
Orlando Pirates yawasha moto kwenye dabi ya Soweto, Simba yapata onyo
4h ago
READ MORE β†’
Manchester United yaendeleza mwenendo mbaya baada ya kichapo kutoka Chelsea
Manchester United yaendeleza mwenendo mbaya baada ya kichapo kutoka Chelsea
5h ago
READ MORE β†’
Gamondi aita kikosi cha kuikabili Nigeria kufuzu Afcon 2027
Gamondi aita kikosi cha kuikabili Nigeria kufuzu Afcon 2027
8h ago
READ MORE β†’
Ligi kuu bara kuendelea leo, Mkwakwani na Isamuhyo kuwaka moto
Ligi kuu bara kuendelea leo, Mkwakwani na Isamuhyo kuwaka moto
10h ago
READ MORE β†’
Dladla awataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao
Dladla awataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao
11h ago
READ MORE β†’
Tunatarajia mchezo mgumu, lakini lengo letu ni ubingwa: Dladla kocha yanga
Tunatarajia mchezo mgumu, lakini lengo letu ni ubingwa: Dladla kocha yanga
11h ago
READ MORE β†’