Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amepanga kukutana viongozi wa Shirikisho la Soka la nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) na Klabu ya Yanga ili kutatua mgogoro unaoendelea kuhusu kusogezwa mbele kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu Machi 24, 2025, kikao hicho kitafanyika jijini Dar es Salaam, Alhamisi na maofisa kutoka Yanga, Simba, TFF na Bodi ya Ligi Kuu wamejulishwa na watahudhuria
"Ni kweli tutakutana na Waziri Kabudi kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo kusogezwa mbele kwa mchezo wetu dhidi ya Simba. Tumepokea barua na tutahudhuria,β alisema afisa mmoja wa Yanga aliyeomba kutotajwa kwa jina
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alithibitisha kikao hicho kitafanyika jijini Dar es Salaam kikiongozwa na Waziri Kabudi. Msigwa pia alieleza maofisa wa Simba watashiriki katika kikao hicho
Mchezo huo, ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliahirishwa baada ya Simba kudai makomandoo wa Yanga waliwakatalia kuingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi yao ya kabla ya mchezo
Simba ilitoa taarifa rasmi kwa Bodi ya Ligi Kuu na TFF, haitoshiriki mchezo huo kwa sababu haki yao ya kufanya mazoezi kabla ya mechi ilikuwa imekiukwa, kama ilivyobainishwa katika kanuni za bodi ya ligi. Kwa upande mwingine, Bodi ya Ligi ilisisitiza mchezo huo ungechezwa kama ilivyopangwa, kulingana na kanuni za ligi.
Hata hivyo, baadaye mchana, bodi ya ligi ilitoa tamko rasmi ikitaja wasiwasi wa Simba na kutaja Kipengele cha 34.1 (1.3) cha kanuni kinachotoa ruhusa ya kuahirisha michezo kwa mazingira ya dharura