Katika dirisha lijalo la usajili linalotarajiwa kuwa na vuguvugu kubwa, klabu ya Yanga SC imehusishwa na mipango ya kumsajili tena kiungo mshambuliaji mahiri, Feisal Salum, maarufu kama "Fei Toto", ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Azam FC.
Feisal alijiunga na Azam FC misimu miwili iliyopita akitokea Yanga SC, katika uhamisho uliotawaliwa na sintofahamu na mgogoro mkali baina yake na klabu hiyo ya Jangwani
Tofauti hizo zilileta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka nchini, huku kila upande ukitoa kauli zenye hisia kali juu ya uamuzi huo.
Hata hivyo, hali imeonekana kubadilika kwa sasa, huku tetesi zikiendelea kuvuma kuwa Yanga SC wanapanga kumrudisha nyota huyo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa
Chanzo cha karibu na uongozi wa klabu hiyo kimeeleza kuwa mazungumzo ya awali tayari yameanza na kuna uwezekano mkubwa dili hilo likakamilika mwez Juni
Feisal Salum amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Azam FC tangu alipojiunga nao, akionyesha kiwango bora, maarifa ya hali ya juu uwanjani, na uwezo wa kuamua mechi.
Umahiri wake katika eneo la kiungo cha ushambuliaji, pasi za mwisho na mabao ya mbali umemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaohitajika mno nchini.
Iwapo atarejea Jangwani, Feisal atakuwa anajiunga na kikosi kilichoimarika zaidi na ambacho kinatafuta mafanikio ya ndani na nje ya nchi. Hii pia itakuwa fursa ya yeye kuandika ukurasa mpya wa historia yake na Yanga, baada ya kuondoka kwa hali ya mvutano miaka miwili iliyopita.
Mashabiki wengi wa Yanga tayari wameanza kuonyesha matumaini na hamasa kuhusu uwezekano wa kurejea kwa fundi huyo, huku wengine wakisubiri kwa tahadhari kuona iwapo uongozi wa klabu utaweza kufanikisha dili hilo.