Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limeeleza kuwa lilitumia muda mwingi kusaidia na kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Wadau wengine ili kuwezesha mechi ya marudiano ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la TotalEnergies CAF 2024/25 kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam tarehe 25 Mei 2025.
Taarifa iliyotolewa CAF mapema leo imebainisha kuwa, ahadi hii ni kwa mujibu wa sera mpya iliyoanzishwa miaka michache iliyopita na Rais wa CAF Dkt. Patrice Motsepe, inayotaka Sekretarieti ya CAF kushirikiana, kusaidia na kufanya kila linalowezekana kwa mujibu wa Katiba ya CAF, Kanuni, utawala na haki, kuhakikisha kila Klabu ya Mpira wa Miguu na Timu ya Taifa katika Nchi 54 Wanachama wa CAF inacheza katika uwanja wa nyumbani uliotambuliwa na unaopendelewa na Viongozi wa Chama cha Soka na Klabu husika.
"Sera hii ni sehemu ya lengo la Rais Motsepe la kuendeleza, kukuza na kustawisha soka la Klabu na Timu za Taifa katika kila moja ya Nchi 54 Wanachama wa CAF na kuchangia katika kuzifanya kuwa na uwezo wa kujitegemea na kujiendesha kifedha kwa uendelevu.
CAF inatoa shukrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais wake Wallace Karia na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania kwa mikutano na majadiliano yaliyofanyika, pamoja na mchango wao na juhudi zao za kusaidia Uwanja wa Benjamin Mkapa kuendana na Kanuni na viwango vya CAF.
Kwa bahati mbaya, kutokana na changamoto za muda, ripoti ya kampuni huru na inayoheshimika kimataifa ya tathmini ya viwanja ilihitimisha kuwa ukarabati na uboreshaji muhimu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa usingeweza kukamilika kwa wakati kwa ajili ya kuandaa mechi ya marudiano ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la TotalEnergies CAF 2024/25 iliyopangwa kufanyika tarehe 25 Mei 2025. Kama ilivyotangazwa awali na CAF katika Taarifa kwa Vyombo vya Habari, mechi ya marudiano sasa itafanyika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
CAF imejizatiti kuendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Serikali ya Tanzania na Wadau wote ili kuhakikisha kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na viwanja vingine vyote, miundombinu na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya uandaaji wa Mashindano ya TotalEnergies African Nations Championship Kenya, Tanzania, Uganda 2024, vinazingatia Kanuni na Viwango vya CAF. Mashindano haya yanatarajiwa kuanza tarehe 2 Agosti 2025 na CAF ina imani kuwa yatakuwa yenye mafanikio makubwa."