Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema amekiandaa kikosi chake kikamilifu kuhakikisha wanashinda mchezo dhidi ya Simba hapo kesho na kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya NBC
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari mapema leo, Hamdi alisema anatambua ugumu wa mchezo huo wa dabi ambao matokeo yake yataamua timu itakayokuwa bingwa wa ligi kuu msimu huu
"Hii ni mechi kubwa inayokutanisha timu kubwa, tunawaheshimu Simba, natambua kesho ni mchezo wa kuamua hatma ya ubingwa Simba au Yanga yeyote anaweza kuwa bingwa, sisi tumejiandaa vyema na natumai tutaweza kupata matokeo mazuri na kutwaa ubingwa kuwapa furaha mashabiki wetu"
"Kila kitu kiko mikononi mwetu, ushindi au hata droo itatosha kutupatia ubingwa lakini Simba lazima washinde kuweza kuwa mabingwa. Bado sijaamua ni mbinu gani tunakwenda kuzitumia katika mchezo huo pengine usiku wa leo au kesho asubuhi tunaweza kuamua. Lakini niwahakikishie Yanga sio timu ndogo, hatuwezi kupaki pasi kumsubiri mpinzani," alisema Hamdi
Akizungumzia hali ya kikosi, Hamdi alisema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo ambapo ni mchezaji mmoja tu Prince Dube ambaye anaweza kukosekana baada ya kupata majeraha katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons
Hamdi amesema kwa kuzingatia changamoto ambazo wamezipitia kwa nyakati tofauti msimu huu, kutwaa ubingwa itakuwa zawadi kuu kwao
"Tumekuwa na maandalizi mazuri, wachezaji wote wako tayari ni Dube (Prince) ambaye ni majeruhi akiendelea vizuri. Aucho na Mudathir hatukuwatumia katika mchezo uliopita kwa sababu wana kadi tatu za njano lakini pia tulifanya 'rotation' katika mchezo uliopita"
"Malengo yetu ni kushinda taji hili na kuwapa furaha mashabiki, huu utakuwa ubingwa wa furaha na heshima kubwa kwetu. Msimu huu tumekumbana na vikwazo vingi, haikuwa rahisi kuweza kufika hapa," aliongeza Hamdi
Licha ya kukiri Simba kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji, Hamdi amesema anafahamu vyema mbinu anazokwenda kuzitumia katika mchezo huo ambao anaamini ubora wa mbinu na utayari wa wachezaji ndio utakaoamua matokeo ya mchezo huo
"Tunajua tunakutana na timu yenye safu nzuri ya ushambuliaji, wachezaji wao watatu wa mbele wanaweza kukufunga wakati wowote lakini najivunia kuwa safu nzuri ya ulinzi inayoongozwa na nahodha wetu Dickson Job na Bacca pamoja na wachezaji wengine"
"Tunajua katika mechi hii tunapaswa kuwa imara katika ulinzi tukiruhusu bao itakuwa tatizo kwetu lakini pia na sisi tukiwafunga bao itakuwa tatizo kubwa kwao, hivyo tunajua ni namna gani tunakwenda kucheza mchezo huu,"