Kikosi cha Simba SC kipo nchini Tunisia ambako leo Jumamosi kitashuka dimbani kumenyana na Esperance de Tunis katika mchezo wa raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kundi D.
Huu ni mchezo unaobeba uzito mkubwa kwa Wekundu wa Msimbazi katika harakati zao za kuendelea kusalia kwenye mbio za kufuzu hatua ya robo fainali.
Hizi ni dakika 90 za kwanza kwa Simba dhidi ya Esperance ugenini, kabla ya timu hizo kukutana tena wiki ijayo jijini Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano. Mechi hizi mbili zitakuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatima ya Simba kwenye kundi D.
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ana kazi nzito ya kuhakikisha timu yake inaondoka na angalau alama nne kutoka mechi hizi mbili. Lengo hilo ni muhimu ili kuweka hai matumaini ya kufuzu robo fainali, hasa ikizingatiwa mwanzo mgumu ambao Simba wameupata kwenye kundi hili.
Ugumu wa mchezo wa kesho unatokana na ukweli kwamba timu zote mbili hazijaanza vizuri kwenye mechi zilizopita. Esperance wametoka sare kwenye michezo yao miwili ya awali dhidi ya Stade Malien na Petro Atletico, wakati Simba wao wamepoteza mechi zote mbili dhidi ya Petro Atletico na Stade Malien, hali inayowaweka kwenye presha kubwa zaidi.
Mchezo wa kesho utakuwa wa pili kwa Esperance kucheza nyumbani, na ikumbukwe kuwa sare yao dhidi ya Stade Malien waliipata kwenye uwanja huo huo.
Kwa Esperance, ushindi ni jambo la lazima ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kusonga mbele, lakini kwa Simba hata sare inaweza kuwa matokeo yenye thamani kubwa, hasa ikizingatiwa mazingira ya ugenini na presha ya mashabiki wa nyumbani.
Ni mechi inayotarajiwa kuwa na presha kubwa na ushindani mkali, ambapo mbinu za kocha Barker, nidhamu ya kimchezo na utulivu wa wachezaji vitakuwa silaha muhimu kwa Simba. Wachezaji wanapaswa kucheza kwa umakini mkubwa, kupunguza makosa na kutumia vyema nafasi zitakazojitokeza.
Kupata matokeo mazuri nchini Tunisia kutakuwa chachu ya kuongeza kujiamini kwa wachezaji kuelekea mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam, ambao Simba italazimika kushinda ili kurejesha matumaini yao kikamilifu.
Baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo, Simba bado ina alama 12 za kuwania katika kundi hili, ambapo kati ya hizo alama sita zipo mikononi mwa Esperance. Dakika 90 za kesho Tunisia zitakuwa mwanzo wa safari ngumu, lakini muhimu, kwa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.