Klabu ya Azam FC imeendelea kuimarisha mwenendo wake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2β0 dhidi ya TRA United, katika mchezo uliochezwa Alhamisi usiku Januari 29, 2026, kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Katika mchezo huo, Azam FC ilionyesha nidhamu ya hali ya juu na umakini mkubwa, huku ikitawala maeneo mengi ya uwanja dhidi ya TRA United waliokuwa wakijaribu kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza.
Jean Ngita aliitangulia Azam FC kwa kufunga bao la kwanza kipindi cha kwanza, akitumia vyema nafasi iliyopatikana ndani ya eneo la hatari. Kipindi cha pili, Idd Nado alihakikisha ushindi wa timu hiyo kwa kufunga bao la pili, lililozima kabisa matumaini ya TRA United kusawazisha.
Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha pointi 16, hatua iliyowasogeza hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na alama sawa na Simba SC, ambayo mapema siku hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 2β0 dhidi ya Mashujaa FC.
Kwa matokeo hayo, ushindani katika nafasi za juu za ligi unaendelea kuwa mkali huku kila timu ikipambana kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea mzunguko unaofuata wa ligi.
Baada ya mchezo huo wa ligi, Azam FC sasa inaelekeza nguvu zake kwenye Kombe la Shirikisho, ambapo itashuka dimbani Jumapili Februari 1, kuvaana na Nairobi United katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex. Mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC katika harakati zao za kuisaka tiketi ya robo fainali.