Mashabiki 45,900 wanatarajiwa kushuhudia mechi ya uamuzi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL) kati ya Al Ahly na AS FAR.
Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri, Jumapili, Februari 15, ambapo Al Ahly itakuwa mwenyeji.
Mamlaka za soka za Misri kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) zimetoa kibali cha idadi hiyo ya mashabiki kuhudhuria mchezo huo kwa kuzingatia sababu za kiusalama, kutokana na ukubwa na ushindani wa mechi hiyo.
Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Al Ahly imetakiwa kutenga tiketi 2,200 kwa ajili ya mashabiki wa AS FAR wanaotarajiwa kusafiri kutoka Morocco hadi Misri kuisapoti timu yao katika pambano hilo.
Al Ahly tayari imejihakikishia tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya CAFCL. Hata hivyo, ushindi au sare katika mechi hiyo utaiwezesha kumaliza kinara wa msimamo wa Kundi B.
Kwa upande wa AS FAR, sare au ushindi utawahakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Matokeo ya ushindi kwa Al Ahly ndio yanayobeba matumaini ya Yanga ya Tanzania kufuzu robo fainali kama itaibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya AS FAR.
Yanga itahitaji kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili kunufaika na matokeo ya ushindi kwa Al Ahly.